Kwanini Rais wa Ukraine havai suti?

Facebook Twitter LinkedIn
Kwanini Rais wa Ukraine havai suti?

Ijumaa ya tarehe 28 Februari haikuwa siku rahisi kwa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alipotembelea ikulu ya White House Marekani.

Kabla hata ya mzozo ulioibuka kati yake na wenyeji wake Rais Donald Trump na Makamu wa Rais JD Vance mbele ya waandishi wa Habari, Trump alimpokea Zelensky mlangoni na kuwaambia waandishi wa habari "leo amevalia kweli kweli"

Baadhi walitafsiri hii si kama sifa bali kijembe kwa Zelensky ambaye alikuwa amevaa fulana nyeusi ya mikono mirefu.

Wakati Trump anampokea Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, alionekana akiyaangalia mavazi ya kiongozi huyo kuanzia juu hadi chini, huku akinong'ona maneno yanayoweza kutafsiriwa kama sifa kwa suti aliyokuwa ameivaa Starmer.

Baada ya malumbano kati ya Zelensky, Trump, Vance, na waandishi wa Habari kukaribishwa kuuliza maswali, mwandishi Brian Glenn kutoka Real America's Voice – chombo kinachoegemea urengwa wa kulia aliuliza kuhusu mavazi ya Zelensky

"Kwanini hauvai suti? Upo katika ofisi ya juu kabisa katika nchi hii, na umegoma kuvaa suti – una suti?" aliuliza Glenn.

Kwa upole, Zelensky alimjibu atavaa suti pale vita vitakapomalizika.

Nitavaa suti vita hivi vitakapomalizika. Labda suti kama yako, labda bora zaidi ya hiyo yako, au labda ya bei nafuu kuliko yako" alisema Zelensky.

Swali hilo la Glenn limeibua mjadala mkubwa mitandaoni huku baadhi wakimuunga mkono mwandishi aliyeuliza huku wengine wakimkosoa kwamba amefanya dhihaka.

Mbunge wa jimbo la Georgia ambaye pia ni mchumba wa mwandishi huyo aliandika katika mtandao wa X kwamba amejisikia fahari kwamba Glenn ameuliza swali hilo.

"Ninajivunia sana @brianglenntv kuonyesha kwamba Zelensky hana heshima kwa Marekani kiasi kwamba hawezi hata kuvaa suti katika Ofisi ya Oval anapokuja kuomba pesa kutoka kwa Rais wetu!!" aliandika Marjorie Taylor Greene.

Hata hivyo mwandishi wa habari machachari kutoka Uingereza na rafiki wa karibu wa Donald Trump Piers Morgan alilikosoa swali hilo na kusema Zelensky si pekee aliyekwenda ofisi ya rais bila kubaa suti. "Swali la kipuuzi. Elon Musk havai suti anapoingia ikulu" aliandika Morgan.

Wanahistoria wanakumbusha pia kwamba Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Winston Churchil aliwahi kufika ofisi ya rais wa Marekani – ijulikanayo kama 'Oval Office' katika ziara rasmi bila ya kuwa amevaa suti.

Tangu kuanza kwa vita nchini Ukraine, Zelensky ameepuka kuvaa suti karibu katika ziara zake za nje ya nchi na hata pale anapokuwa ametembelea na viongozi mbalimbali kutoka nje ya nchi yake.

Tangu nchi yake kuvamiwa na Urusi mwaka 2022, Zelensky amekuwa akipendelea kuvaa aidha tisheti na suruali ya kijeshi zote zikiwa za kijani kibichi au vya rangi nyeusi kama aliyokwenda nayo ikulu ya marekani.

Zipo tafsiri kadhaa zilizotolewa juu ya aina ya vazi analopendelea kuvaa hivi sasa Zelensky ikiwa ni pamoja na kutoa ishara ya hali tete na ya dharura inayoendelea nchini mwake

Sababu nyingine inasemwa ni ujumbe wa mshikamano ambao Zelensky anauonyesha kwa wanajeshi wa nchi yake walio mstari wa mbele wa mapambano.

Lakini pia Zelensky anataka kutuma ujumbe kwamba yeye si kiongozi anayevaa suti, na kuongoza nchi yake kwa mbali, bali ni kiongozi anayeshiriki moja kwa moja katika mapambano ya kuilinda nchi yake

Hata kabla ya uvamizi wa Urusi nchini mwake, akiwa kiongozi aliyetokea katika fani ya ucheshi na si mwanasiasa wa kawaida, Zelensky anaelezwa kupendelea Kwenda tofauti na mazoea ya siasa si tu katika mavazi yake lakini hata katika namna anavyoiongoza.

admin

admin

Content creator at LTD News. Passionate about delivering high-quality news and stories.

Comments

Leave a Comment

Be the first to comment on this article!
Loading...

Loading next article...

You've read all our articles!

Error loading more articles

loader