Dakika 10 za majibizano kati ya Trump na Zelensky katika Ikulu ya Marekani

Facebook Twitter LinkedIn
Dakika 10 za majibizano kati ya Trump na Zelensky katika Ikulu ya Marekani

Rais wa Ukraine alikuwa na matumaini chanya ya kuondoka katika Ikulu ya White House Ijumaa baada ya mazungumzo chanya na Donald Trump, ambayo yangekamilika kwa kusainiwa kwa makubaliano ya madini ambayo yangeipatia Marekani umiliki katika mustakabali wa Ukraine, ingawa si hakikisho la usalama kamili kwa Ukraine.

Badala yake, Volodymyr Zelensky alikabiliwa na manemo makali mbele ya vyombo vya habari vya kimataifa, baada ya Rais Trump na Makamu wake Rais JD Vance kudai shukrani zaidi kwa msaada ambao Marekani imetoa kwa miaka mingi.

Rais wa Ukraine alijibu mapendekezo kutoka kwa washirika wake hao wenye nguvu zaidi kwamba anapaswa kufanya juhudi zaidi ili kukubaliana na Vladimir Putin kuhusu kusitisha mapigano. Walimjibu kwamba alikuwa "akidhihaki".

Zelensky alielekezwa hatimaye kuondoka Ikulu ya White House mapema kabla yeye na Trump hata kufanya mkutano wa waandishi wa habari kama ilivyoratibiwa.

Na mkataba wa madini, ambao ulikuwa ukitangazwa na kupigiwa upatu na pande zote mbili wiki hii, haukusainiwa.

"Rudi wakati utakapokuwa tayari kwa ajili ya mchakato wa amani," Trump aliandika kwenye mtandao wa kijamii kabla ya gari la Zelensky kuondoka.

Kulikuwa na maeneo kadhaa ya mivutano mikubwa katika mkutano huo.

Hapa tunaangazia maeneo manne;

1) Hasira zawapanda Zelensky na Vance

Katika nusu saa ya mazungumzo ya amani na taratibu mwanzoni, mvutano ulianza kuzidi katika Ofisi ya rais wakati Vance aliposema "njia ya amani na ya mafanikio ni kushiriki katika mchakato wa kidiplomasia".

"Hicho ndicho anachofanya Rais Trump," alisema.

Zelensky aliingilia kati, akirejelea uchokozi wa Urusi katika miaka ya kabla ya uvamizi wake rasmi miaka mitatu iliyopita ikiwa ni pamoja na kushindikana kwa usitishwaji mapigano 2019.

"Hakuna aliyemzuia," alisema akimaanisha rais wa Urusi Vladimir Putin.

"Diplomasia gani hiyo JD unayoizungumzia? Unasemaje?" Alisema.

Majibizano hayo yakawa ya wasiwasi, na Vance akajibu: "aina ambayo itamaliza uharibifu kwa nchi yako."

Makamu huyo wa rais alimshutumu Zelensky kwa kukosa heshima na "kudai" hivyo mbele ya vyombo vya habari vya Marekani.

Ilikuwa ni utetezi wa Vance juu ya mbinu ya Trump ya kumaliza vita - kwa kuanzisha mazungumzo na Putin na kushinikiza kusitishwa kwa haraka kwa mapigano - ambayo awali ilizidisha mvutano na kiongozi huyo wa Ukraine.

2) 'Usitueleze tutajisikiaje'

Baada ya Vance kumkosoa rais wa Ukraine kuhusu changamoto za jeshi lake, Zelensky alijibu: "Wakati wa vita, kila mtu ana matatizo, hata wewe. Lakini una fursa nzuri lakini huioni sasa utaihisi katika siku zijazo."

Maoni hayo yalimpa nafasi Trump kuingilia na kumleta kwenye majibizano ambay hadi wakati huo yalikuwa kati ya Zelensky na makamu wa rais.

Hapa alikuwa kiongozi wa Ukraine akieleza Trump ameshindwa kufahamu hatari ya kimaadili ya kushirikiana na mwanzilishi wa vita.

Ujumbe wa Zelensky ulikata kiini cha kile ambacho wakosoaji wanasema ni makosa ya kimsingi ya Trump katika kushughulika na Urusi.

Kwamba kwa kuikingia kifua Moscow iliyotengwa na kutafuta usitishaji vita haraka anahatarisha kumtia moyo Putin, kudhoofisha Ulaya na kuiacha Ukraine katika hatari.

Trump amekuwa akiashiria kwamba vita ni aina ya mzozo kati ya pande mbili ambazo zinapaswa kuwajibika kwa lawama na chanzo chake.

Lakini Zelensky alikuwa akijaribu kuonya juu ya matokeo mabaya ya mtazamo huu.

Kiongozi wa Ukraine akamwambia Trump moja kwa moja katika Ofisi ya rais: Ifurahishe Urusi, na vita vitakuja kwako.

Kauli iliyoamsha hasira ya Trump ;"Usituambie tutajisikiaje.Huna uwezo wa kutuambia hivyo," alisema, sauti yake ikiongezeka.

"Huna nafasi sasa hivi," alimwambia. "Unacheza kamari na maisha ya milioni ya watu."

Majibizano haya yanaweza kumpa sifa Zelensky miongoni mwa wale waliotaka kumuona akimpinga Trump; lakini wakati huu pia unaweza kuamua mustakabali wa vita na amani ya Ulaya.

3)'Haujawahi kuwa peke yako'- Trump

Katika moja ya hatua za mazungumzo hayo, Zelensky alisema: "Tangu mwanzo wa vita, tumekuwa peke yetu na tunashukuru."

Hii ilimkasirisha Trump, ambaye mara kwa mara ameelezea vita hivyo kama mzigo kwa walipa kodi wa Marekani.

"Haujawahi kuwa peke yako," alisema. "Haujawahi kuwa peke yako. Tulikupa $350bn kupitia rais huyu mpumbavu - ," akimrejelea Biden.

Kisha Vance akamuuliza Zelensky ikiwa alikumbuka kushukuru Marekani wakati wa mkutano na kumtuhumu kwa kufanyia kampeni upinzani yaani Democrats kipindi cha uchaguzi mkuu wa Marekani mwaka jana.

Maoni hayo yalirejelea ziara aliyofanya Zelensky kwenye kiwanda cha silaha huko Scranton, Pennsylvania - mji wa kwao Joe Biden - wiki chache kabla ya Wamarekani kupiga kura katika uchaguzi wa Novemba.

Wana-Republican walikasirishwa na ziara hiyo, wakimtuhumu Zelensky kwa kubadilisha ziara hiyo kuwa tukio la kampeni la kisiasa akimpendelea Kamala Harris katika jimbo hilo lenye ushindani.

Hapa ndipo mgawanyiko mkali wa siasa za ndani za Marekani ulipoibuka katika wakati muhimu kwa usalama wa dunia.

"Tafadhali, unadhani kwamba ikiwa utazungumza kwa sauti kubwa kuhusu vita," Zelensky alianza kusema, lakini Trump akamkatiza.

"Yeye hasemi kwa sauti kubwa," Trump alijibu, akiwa waziwazi ameudhika. "Nchi yako iko katika shida kubwa."

"Hamshindi, hamna ushindi hapa," Trump alisema. "Una nafasi nzuri ya kutoka salama kwa sababu yetu."

4) Zelensky anajibu - kwa gharama gani?

"Jambo hili litakuwa gumu sana," alisema Trump. "Itakuwa makubaliano magumu kufanyika kwa sababu mitazamo inahitaji kubadilika."

Rais na makamu wa rais walimkosoa Zelensky, na kuonekana kukasirishwa zaidi na kile walichodhani kama "tabia yake binafsi."

"Semeni asante tu," alidai Vance.

Majibu ya Zelensky - ambayo yalikuwa ya kuthibitisha uhalisia kwa wanaume hao wawili wenye nguvu zaidi - yalionekana kuendeshwa na hali ya kipekee wakati huu.

Amekuwa akijitetea kwa miaka mitatu akilinda nchi yake dhidi ya uvamizi, huku pia akijaribu kuimarisha jamii na uongozi wa kisiasa ambao Putin amejitahidi kuusambaratisha.

Lakini kando na kamera kuu, kulikuwa na picha nyingine katika chumba hicho.

Balozi wa Zelensky mjini Washington, Oksana Markarova, alionekana akiwa ameweka mikono kichwani wakati mvutano ulipoongezeka.

Hii ni taswira inayoelezea hali ya kidiplomasia ya Zelensky na uhusiano wake na mdhamini wake mkubwa katika jitihada za kumkabili Putin.

Kusimama mbele ya Trump kama alivyofanya Ijumaa, inaweza kumaanisha kushindwa mbele ya Putin.

admin

admin

Content creator at LTD News. Passionate about delivering high-quality news and stories.

Comments

Leave a Comment

Be the first to comment on this article!
Loading...

Loading next article...

You've read all our articles!

Error loading more articles

loader